Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu amefunguka na kuwashukuru Watanzania mbalimbali ambao wamekuwa na yeye katika maamuzi magumu aliyofanya kuachana na CCM pamoja na kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge kupitia chama hicho.
Nyalandu amesema kuwa hoja zilizopo mbele kwa sasa ni kubwa kuliko mtu mmoja mmoja na zinalenga kuleta utashi kwa kila Mtanzania kutafakari na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuendeleza nchi katika Demokrasia, uchumi na kijamii.
"Nachukua nafasi hii kumshukuru kila mmoja wetu ayenitumia salaam na kuunga mkono hatua niliyochukua.
Hoja zilizombele yetu ni kubwa kuliko mtu binafsi mmoja mmoja, na zinalenga kuhuisha utashi wa kila Mtanzania kutafakari na kushiriki kikamilifu safari ya kuiendeleza nchi yetu Kidemokrasia, kiuchumi, na kijamii.
Ni maombi yangu kuwa, ujasiri ukaondoe roho ya woga, upendo uondoe chuki, nia njema iondoe kuoneana, na kweli ituweke huru na iondoe roho ya kusingiziana kunakoleta kuumizana na sintofahamu ya hali ya juu.
Ikawe Heri kwa Watanzania wote" aliandika Nyalandu
Mbali na hilo Lazaro Nyalandu amekanusha taarifa inayosambazwa ikionyesha kuwa alikuwa ana chat kupitia kundi la Whatsapp na baadhi ya viongozi wa CHADEMA akiomba akionyesha kuwa alifanya madhambi wakati akiwa Waziri wa Maliasili na kusema huo ni uzushi wa kutungwa na kusema ni siasa za kizamani hizo.
"Habari hii ni ya kutungwa na ni uzushi! Sijawahi kuwa kwenye GROUP hili la kutunga wanaloliripoti. siasa za kuzushiana mambo sio za kistaarabu na ni za kizamani.
Aibu kwani waongo wote sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto na kiberiti. Tuwapuuze" alisisitiza Nyalandu.
Comments
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA