KUTOKA KWA RAISI MAGUFULI MAJIZI YA CCM KUHAMIA CHADEMA

Rais Magufuli amesema yalikuwapo majizi CCM kuliko hata ya Chadema na wengine wametoka kwenye chama hicho tawala na kukimbilia chama hicho cha upinzani.

Alisema pia kuwa wapo waliopo Chama cha Wananchi (CUF) wengine ni wabaya sana.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Mkuyuni jijini Mwanza.

“Ndiyo maana tumeamua kuijenga reli ya umeme na sio ya kuendeshwa na dizeli kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa fedha za ndani za Watanzania Sh trilioni 7, nataka niwaambie kwamba hata kama itachukua miaka 10 itafika Mwanza na speed (mwendo kasi) yake ni kilomita 160 kwa saa.

“Tunataka Tanzania mpya, hilo ndiyo lengo langu na ndiyo maana nilipofika hapa sikusema CCM oyee kwa sababu yapo yaliyokuwepo CCM yalikuwa majizi sana kuliko hata ya Chadema.

“Ndiyo maana mimi niko hapa sijasema Chadema oyee, kwa sababu yalikuwepo majizi CCM yakakimbilia Chadema, ndiyo maana sijasema CUF oyee, kwa sababu wapo waliopo CUF wengine ni wabaya sana, mimi nataka maendeleo, nasema Tanzania oyee, kwa sababu Tanzania inatakiwa kujengwa na Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alishangazwa na kutokuwapo na hata kiwanda cha drip, mabomba ya sindano na pampas hapa nchini, huku vyote vikiagizwa kutoka mataifa mengine.

“Hata mimi mwenyewe najua kutengeneza maji ya drip, wanafunzi wa chuo waliosoma kemia kwa kidato cha nne na sita wanajua kutengeneza, kwanini tusitengeneze maji ya drip badala yake tunanunua Uganda? Tunashindwaje kuwatumia wanafunzi au wahitimu wa kemia kutengeneza?” alihoji.

Pia alitoa angalizo kwa mwekezaji wa Kiwanda cha nguo cha Mwatex kilichopo Mwanza, kuhakikisha kinaongeza uzalishaji na kuacha visingizio na kama ameshindwa ni vema kukiachia ili kukabidhiwa mtu mwingine.

Rais Magufuli alionyesha pia kushangazwa na mwekezaji wa kiwanda hicho, kupewa kingine Mbeya na sasa hakifanyi kazi ipasavyo.

Aunga Mkono Juhudi za Wananchi
Akiwa kiwandani hapo, Rais Magufuli alitoa Sh milioni tatu kwa lengo la kununulia mifuko 100 ya saruji kwa shule mbili zilizopo ndani ya kata hiyo.

Rais Magufuli alimkabidhi fedha Diwani wa Kata ya Igogo, John Minja, akiunga mkono juhudi za wananchi wa kata hiyo katika kuboresha miundombinu.

Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, alimweleza Rais Magufuli kuwa wananchi wa kata hiyo wamechanga Sh milioni 15.8 kujenga matundu ya vyoo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwa aliwahi kuishi ndani ya kata hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Victoria Moulders & Polybags, Manjist Singh, alisema bidhaa zinazozalishwa hapo zinauzwa Uganda, Rwanda, Burundi na ndani ya nchi na kuongeza kuwa alikianzisha kutokana na uwepo wa shughuli za kilimo na madini.

Hata hivyo, aliomba Serikali kupunguza matatizo yaliyopo soko la ndani kwa kuondoa utegemezi wa bidhaa za nje kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji wa ndani.

Comments