BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu sana tujifunze neno la MUNGU la kutuvusha.
Leo tunaitazama imani Pekee ya uzima wa milele. Imani ya pekee ya kuwapeleka watu uzima wa milele ni imani ya KRISTO pekee.
"Warumi 10:17 '' Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.''
-Kwa sababu njia ya uzima ni moja tu yaani KRISTO YESU, tunatakiwa tubaki siku zote katika njia hii ya uzima.
-Imani ya KRISTO ni njia ambayo sio wote wanaiona lakini kwa wale ambao wameiona imani hii ya uzima nina neno kwao leo.
Wateule: Ni Vizuri Sana Kuipalilia Amani Yako Ya Uzima Katika KRISTO YESU.
"Yuda 1:20-25 '' Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya BWANA wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele.
Wahurumieni wengine walio na shaka,
na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili. Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu; Yeye aliye MUNGU pekee, Mwokozi wetu kwa YESU KRISTO BWANA wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina.''
=Kuna Mambo 8 Ya Kufanya Ili Imani Yako Iwe Hai.
1. Imani Inapaliliwa Kwa Maombi.
Zaburi 116:1-2 ''Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.''
-Maombi hufanya kila kitu kuwa rahisi, maombi hufanya kwenda ibadani kuwa sio mzigo bali faida kuu.
-Maombi hutufanya tuwe imara katika imani yetu iliyo kuu sana.
-Maombi hutufanya kila kitu kinachohusika na imani yetu kuwa rahisi, ukiona mtu anachoka huyo kwanza amepungukiwa maombi na ucha MUNGU.
Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''
2. Imani inapaliliwa kwa Kumsifu Na Kumwabudu MUNGU.
Zaburi 150:1-6 '' Haleluya. Msifuni MUNGU katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake.
Msifuni kwa matendo yake makuu; Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake. Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi; Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi; Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana. Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Haleluya''.
-Kumsifu MUNGU huambatana na kumwabudu, Kuna nyimbo nyingi za kuabudu lakini zinaonyesha matendo makuu ya MUNGU hivyo huko ni kumsifu na kumwabudu MUNGU.
-Kumsifu MUNGU ni kukuweka huru katika kumwabudu MUNGU na kukufanya pia uwe imara katika imani yako.
-Kumwabudu MUNGU ni kumpa heshimu kuu muumba ambaye hakuna aliye kama yeye.
-Kwa njia ya kumsifu na kumwabudu MUNGU kutakufanya kuwa karibu na MUNGU na kuwa imara katika imani yako.
3. Imani inapaliliwa kwa Kusoma Neno La MUNGU Kulitafakari Na Kulitendea Kazi.
“Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.” (Yakobo 1:22-24).
-Neno la MUNGU ndio uhakika wetu na dira yetu ya maisha yetu ya duniani na maisha baada ya kuondoka duniani.
-Neno la MUNGU ndilo linaloongoza kwa kutufanya tuwe imara katika imani.
-Neno la MUNGU hatutakiwi kulisoma tu bali kulisoma, kulitafakari na kutendea kazi kile tulichosoma, huko ndiko kupalilia imani yetu.
4. Kujitakasa.
1 Thesalonike 4:3-5 ''Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU ''
-baada ya kutakaswa dhambi zako zote kupitia YESU KRISTO unatakiwa uishi maisha ya utakaso. Maisha ya utakaso hayana muda fulani bali ni maisha ya kudumu.
-Kwa sababu imani yetu ni takatifu sana na inataka tuwe watakatifu kama atakavyo BWANA aliyetuokoa; Kudumu kwetu katika utakatifu huo ni kuipalilia imani maana mtakatifu hujiamini na ana uhakika. utakosa uhakika wa uzima wa milele kama tu wewe hutaishi maisha matakatifu.
5. Kujumuika Pamoja Na Watakatifu Wengine.
Mithali 13:20 '' Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.''
-Wenye hekima hawa wanaozungumzwa hapa ni wale wenye elimu ya MUNGU kupitia KRISTO YESU. Kama imani yako ni changa kwa kujumuika na walio na imani thabiti kuliko wewe itakusaidia kukua kiimani.
-Kupitia watakatifu wengine utajifunza mambo mengi ya ki-MUNGU ambayo yatakusaidia katika kukua kwako kiimani.
6. Kumsikiliza ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.' '
-ROHO MATAKATIFU ndiye msimamizi wa wokovu wetu.
-ROHO MATAKATIFU ndiye mwangalizi wa imani yetu.
-Ukitaka kukua kiimani lazima uwe unamsikiliza ROHO MATAKATIFU maana yeye ndiye anayejua yote.
Kumkataa ROHO MTAKATIFU ni kuikataa imani ya uzima.
Kumkataa ROHO MTAKATIFU ni kumkataa YESU KRISTO na kumkataa YESU KRISTO ni kumkataa MUNGU muumbaji wa vyote.
Kwa sababu wakristo wanatakiwa waishi kwa ROHO MTAKATIFU hivyo hivyo wanatakiwa waenende kwa ROHO MAKATIFU na hapo imani yao lazima ikue tu.
7. Kumtii KRISTO.
Yohana 15:4-6 '' Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.
Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. ''
-YESU KRISTO ndiye mti na sisi ni matawi ya huo mti. huwezi kujiita mkristo harafu humtaki KRISTO wewe utakuwa mpinga KRISTO na hakuna mpinga KRISTO hata mmoja anayeweza kuingia uzima wa Milele.
-Tawi lazima liwe katika Mti na tawi haliwezi kwenda kinyume na mti maana kukua kwa tawi na kustawi kunategemea mti wenyewe. Sasa wewe kama tawi ni lazima umtii BWANA YESU maana Hakuna Ukristo bila KRISTO, na Ukristo sio dini bali ni kuishi maisha ya Wokovu katika KRISTO.
8. Kuitenda Kazi Ya MUNGU.
Zaburi 100-:2 '' Mtumikieni BWANA kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba;''
-Kumtumikia MUNGU ni njia ya kuwa karibu na MUNGU.
-Kumtumikia MUNGU kutakufanya usiwe na hofu wala woga bali imani yako itakuwa inaimarika siku hadi siku.
Huku Unapalilia Imani Siku Zote, Kumbuka Pia Kuilinda Imani Yako Ili Isivamiwe Na Imani Za Kishetani, Mila Na Desturi.
Tengeneza Imani Yako Na Enenda Kwa Imani Siku Zote
2 Kor 5:17 ''
Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''
BWANA YESU Anakupenda Sana Na Anakuandalia Makao Mbinguni,
-Dumisha Tu Utakatifu, Kujikana Na Kujitoa.
-Kataa Dhambi, Ogopa Dhambi, Ikimbie Dhambi Na Usifanye Dhambi.
-Usiyumbishwe Na Vinavyoonekana Bali Waza Uzima Wa Milele Ambao Haupatikani Kwingine Kokote Ila Kwa BWANA YESU
Waefeso 2:8 '' Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; ''
-Waache Wanaong'ang'ania Dhambi Waendelee, Wewe Mche MUNGU. Waache Wazinzi Na Waasherati Waendelee Na Uchafu Wao, Wewe Endelea Kujitakasa Na Maombi. Waache Waabudu Sanamu Na Sanamu Zao, Wewe Itii Biblia. Waache Wasoma Nyota Na Nyota Zao, Wewe Funga Na Kuomba. Waache Wanaokataa Kuokoka Waendelee Na Mawazo Yao, Wewe Sema YESU Ni BWANA. Waache Wanaomkataa YESU Leo Kwa Sababu Tamaa Zao, Wewe Shikilia Wokovu Kama Pesa, YESU Amekuweka Huru Mbali Dhambi .
Yohana 8:36 '' Basi Mwana(YESU) akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. ''
-Siku Ya Mahesabu I Karibu Na Siku Hiyo Kila Mtu Atavuna Sawasawa Na Anavyopanda Sasa.
BWANA YESU anasema
''Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.
Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Ufunuo 22:11-12''
-Urafiki Na Dunia Ni Kujiangamiza, Waliookoka Sasa Wanaonekana Kama Watu Duni, Ni Kama Wamechanganyikiwa Maana Wao Hawajishughurishi Na Ukisasa Wa shetani, Wateule Hata Hawajui Madawa Ya Kulevya, Hawajuia Kuna Jipya Gani Kwenye Miziki Ya Kidunia, Hawa BWANA MUNGU Anawapenda Sana. Kadiri Duniani Inavyowachukia Wateule Ndivyo Mbingu Za Mbingu Zinawapenda Sana. BWANA Yu Karibu Ndugu na kumbuka wewe mtenda dhambi kwamba Baada Ya Kifo Ni Hukumu.
- Huu Ni wakati Wa Kutubu Maana Ufalme Wa MUNGU Umekaribia(Mathayo 3:2 )
Tena Ni Wakati Wa Kuutafuta Ufalme Wa MUNGU Na Haki Yake Ndipo Hayo Mengine Tunayoyataka Tutazidishiwa(Mathayo 6:33 ).
Kama Huwezi Kuwa Karibu Na MUNGU Huwezi Kupata Ufunuo Kutoka Kwa MUNGU.
Ndugu uliye na KRISTO hakikisha unapalilia imani yako kila siku na hakikisha unailinda imani yako iliyo ya thamani sana.
Ndugu ambaye bado hujampokea YESU hakikisha unampokea na kuanza kuipalilia imani yako katika KRISTO ambayo ni ya thamni sana.
Yuda 1:3 '' Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. ''
-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu
KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.
''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu ''
BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu.
BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10.
BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.''
Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
Comments
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA