Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mchungaji Peter Msigwa amefunguka na kuonyesha nia yake ya kutaka kumuondoa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai iko pale pale.
Mchungaji Msigwa mwezi Oktoba 2017 alionyesha nia ya kupeleka hoja Bungeni ili kumuondoa Spika Job Ndugai katika nafasi yake hiyo na kusema atatumia kanuni za Bunge na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya hivyo kwa kile anachoamini kuwa Spika wa Bunge ameshindwa kusimama vyema katika nafasi hiyo jambo ambalo limepelekea Bunge hilo sasa kuonekana halina nguvu na kushindwa kuisimamia serikali.
Msigwa amesema kuwa anaamini kuwa wabunge mbalimbali ambao wana akili wataungana na hoja yake hiyo ya kutaka kumuondoa Spika Job Ndugai katika kiti hicho kwa kutumia kanuni za Bunge na Katiba ya nchi.
“Hoja ya kumung’oa spika iko pale pale! Naamini wabunge Wenye akili wataiunga mkono” aliandika Mbunge Msigwa kupitia mtandao wake wa Instagram
Wabunge mbalimbali wa upinzani wamekuwa wakitoa lawama kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa linashindwa kuisimamia serikali ipasavyo na wengine wamekuwa wakidai kuwa Bunge hilo linaendeshwa na serikali, jambo ambalo limemfanya Mbunge Msigwa kutaka kupeleka hoja ya kumuondoa kiongozi wa Bunge hilo Spika Job Ndugai.
Comments
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA