ASKARI WA KIKOSI CHA FFU AMUUA MKE WAKE KWA MADAI YA TUMIZI LA MTOTO

Polisi wilayani Babati mkoani Manyara inamshikilia askari wa jeshi hilo Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Cosmas James akituhumiwa kumuua mzazi mwenzake, Regina Daniel (23) kwa kumpiga risasi nne.

Chanzo cha mauaji hayo inadaiwa ni mzozo ulitokea Regina alipomfuata James lindoni kudai fedha za matumizi ya mtoto.
Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Longinus Tibishubwamu amesema lilitokea mjini Babati Ijumaa Oktoba 27,2017 saa 12:30 jioni.

Amesema askari huyo alikuwa lindoni katika Benki ya NMB tawi la Babati, mtaa wa Usalama, Kata ya Bagara.
Kaimu Kamanda Tibishubwamu amesema Regina ni mkazi wa Mtaa wa Ngarenaro mjini Babati.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kabla ya kifo cha mwanamke huyo kulitokea mzozo kati ya wawili hao kuhusu fedha za matumizi ya mtoto.

"Wakati wakiendelea na mzozo, ndipo askari huyo kwa kutumia silaha aliyokuwa nayo alimpiga Regina risasi nne kwenye paji la uso, kifuani na shingoni," amesema.

Amesema askari huyo alitumia silaha aliyokuwa nayo lindoni aina ya SMG mali ya Jeshi la Polisi.

Baada ya tukio, amesema askari huyo aliitelekeza silaha lindoni na kwenda kujisalimisha polisi. Amesema askari waliokwenda eneo la tukio waliokota maganda matatu ya risasi na waliichukua silaha hiyo.

Kaimu Kamanda Tibishubwamu amesema mtuhumiwa yupo mahabusu kwa mahojiano kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mji wa Babati ya Mrara.

Askari wa FFU mjini Babati, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema anashangazwa na tukio hilo kutokana na upole alionao James.
Amesema James ni askari mwenye nidhamu, hivyo hafahamu jambo gani limempata hadi akamuua mzazi mwenzake.

Comments