WATANZANIA WOTE KUWA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA IFIKAPO DISEMBA 2018


MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza kuandikisha, kusajili na kuwatambua wananchi wa kuwapa Vitambulisho vya Taifa katika mikoa 12 ikilenga kutoa vitambulisho hivyo kwa Watanzania wote wanaostahili ifikapo Desemba 2018.

Akizungumza kwa simu, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Andrew Massawe jana aliitaja mikoa ambayo tayari imefikiwa na mamlaka hiyo kuwa ni Dodoma, Mbeya, Njombe, Songwe, Singida, Simiyu, Geita, Mwanza, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Iringa.

Pamoja na mikoa hiyo, mamlaka hiyo pia kesho inatarajia kuzindua usajili wa wananchi kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho hivyo mkoani Mtwara. 

Alisema wanashirikiana na Wakala wa Ufilisi, Usajili na Udhamini (RITA), Idara ya Uhamiaji na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili kuhakikisha kila mwananchi anayepatiwa kitambulisho amekidhi sifa ya uraia wake.

Alisema baada ya NIDA kutoa fomu na kusajili itaingia hatua ya utambuzi kwa kubandika majina ya wananchi waliojitokeza kujisajili ili kutoa fursa wananchi kutambua watakaotumia fursa hiyo kujipatia kitambulisho hicho bila kuwa na sifa.

Alisema baada ya kukamilisha utambuzi, taarifa zote zilizokusanywa katika mikoa hiyo 12, zitawasilishwa makao makuu Dar es Salaam kutolewa vitambulisho na mamlaka hiyo itatoa namba za utambulisho kwa wananchi waliopitia michakato yote.

Alisema hadi kufikia Juni mwakani, wananchi wote waliopo nchini wenye sifa na wanaostahili kupatiwa vitambulisho hivyo vya taifa watakuwa wameshapatiwa namba ya utambulisho na ifikapo Desemba mwaka huo, watakuwa wamepata vitambulisho.

Mkurugenzi huyo alisema, kutolewa kwa vitambulisho hivyo ni utaratibu endelevu kwa kuwa kila mwananchi aliyefikisha umri wa miaka 18 atapata kitambulisho hicho. 

Alitaja vitu ambavyo mtu anatakiwa awe navyo kukidhi vigezo vya vitambulisho hivyo kuwa ni kuwa na cheti cha kuzaliwa na endapo hana cheti hicho ni lazima uhamiaji imthibitishe, cheti cha kitaaluma, kadi ya kupigia kura au hati ya kusafiria.

Comments