Radi imeua ng’ombe 10 na kumvua mwanamke koti alilovaa katika kitongoji cha Itandora wilayani Tarime mkoani Mara.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Elias Matto alisema kutoka Tarime jana kwamba ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:30 jioni nyumbani kwa Joseph Chacha maarufu kwa jina la Tuelewane.
Alimtaja mwanamke aliyevuliwa koti na radi kuwa ni Rhobi Joseph, mke wa Chacha; wamiliki wa ng’ombe waliouawa wenye thamani ya Sh milioni tatu.
Matto alisema ajali hiyo ilitokea wakati mvua ikinyesha na radi ilianza kumvua Rhobi koti alipokuwa akijiandaa kupika chakula cha usiku ndani ya nyumba yao kabla ya kuua ng’ombe hao wakiingia zizini.
“Baada ya kuvuliwa koti likatupwa chini, huyu mama alipata mshituko na baadaye alihisi maumivu ya kichwa na kiuno ingawa yaliisha baada ya dakika chache,” alieleza kiongozi huyo wa kitongoji hicho.
Matto alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea huko na ng’ombe hao 10 ni kati ya 60 wa familia hiyo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kibasuka kilipo kitongoji hicho, Mwita Mtatiro alithibitisha ajali hiyo.
Alisema ng’ombe waliouawa walitarajiwa kufukiwa ardhini jana ili kuepusha madhara kwa jamii.
IMEANDIKWA NA CHRISTOPHER GAMAINA-Habarileo
Comments
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA