RAISI MAGUFULI APIGA MARUFUKU BOMOA BOMA JIJINI MWANZA

Rais John Magufuli ameagiza kusitishwa kwa ubomoaji wa nyumba za wananchi zaidi ya 2,000 wanaodaiwa kuvamia eneo la Uwanja wa Ndege Mwanza, kituo cha polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ).

Akizungumza na wananchi wakati uzinduzi wa daraja la juu la waenda kwa miguu eneo la Furahisha jijini Mwanza leo Jumatatu, Rais Magufuli ameagiza ubomoaji huo usitishwe hadi atakapotolea uamuzi suala hilo.

“Rais ndiye msimamizi mkuu na mwenye mamlaka juu ya ardhi yote nchini; hawa (wananchi) ndio walionipa urais," amesema Rais Magufuli.

Agizo la Rais Magufuli anayefanya ziara ya siku mbili mkoani Mwanza limetokana na mabango ya wananchi kutoka maeneo ya Kayenze, Muhoze na Kigoto wakielezea kero zinazowakabili ikiwemo tishio la nyumba zao kubomolewa kwa madai ya kuvamia maeneo ya ndege, jeshi la polisi na JWTZ

Rais amewaagiza mawaziri wanne kutoka Wizara za Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mambo ya Ndani, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kukutana kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kutatua mgogoro huo ndani ya siku 21 kunazia leo Jumatatu.

Amesema baada ya mapendekezo ya vikao vya mawaziri hao, ataangalia namna ya kushughulikia suala hilo, hata kama itabidi kubadilisha sheria kulinda maslahi ya wananchi ambao baadhi wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 30.

Katika hotuba yake, Rais pia ameahidi kukamilisha malipo ya Sh9 bilioni yanayodaiwa na mkandarasi anayetekeleza mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa kiwango cha kimataifa ili ukamilike kabla ya mwaka 2020.

Comments