UJENZI wa njia sita katika barabara ya Morogoro yenye kilomita 16 kutoka Kimara, Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani, unatarajiwa kuanza mwisho wa mwezi huu, imebainika.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale, alisema hayo alipokuwa akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipotembelea na kukagua ubomoaji wa majengo ya serikali likiwamo jengo la Shirika la Umeme (Tanesco) na nyumba za watu zilizoko eneo la barabara ili kupisha mradi huo.
Mfugale alisema kazi inayofanyika kwa sasa ni ubomoaji wa majengo na nyumba kuanzia Kimara hadi Kiluvya na kwamba ujenzi utaanza mwisho wa mwezi huu.
Pia alisema ujenzi huo utafanywa na mkandarasi atakayepatikana na atapewa mapendekezo ya serikali ambavyo inataka ujenzi wa barabara hizo uwe na yeye ataona kama inafaa kwa ajili ya kuhakikisha ujenzi unakuwa wa kisasa.Sambamba na hilo, alisema ukarabati wa daraja la Mbezi ambalo lilikatika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Novemba, mwaka huu, unaendelea na hadi kukamilika utagharimu Sh. milioni 650.
Alisema mvua hizo pia zilianza kumega barabara hali ambayo ingesababisha usumbufu kwa watumiaji.Mfugale pia alisema mbali na ujenzi wa njia hizo, mradi huo pia utahusisha ujenzi wa madaraja mengine makubwa na ya kisasa katika maeneo ambako yatahitajika.
Waziri Mbarawa, mbali na kuipongeza Tanesco kwa kazi nzuri na kubwa inayoendelea ya kubomoa jengo lake, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha barabara hizo zinajengwa ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Akiwa eneo la Kimara Temboni, aliwaeleza wananchi kuwa mbali na njia hizo sita, pia wamejenga barabara ya mtaani kwa kiwango cha lami itakayotokea Kimara mwisho na kuendelea kupunguza msongamano barabara kuu.
“Tutajenga na barabara hii ya mtaani ambayo kwanza itasaidia wananchi wengine wasiingie eneo la barabara na kuanza kujenga lakini pia itawarahisishia shughuli zenu wakazi wa maeneo haya kwa sababu itatokea Kimara Mwisho.
Lengo la serikali ni kuwarahisishia maisha wananchi kwa kuondokana na adha kubwa ya usafiri waliyokuwa wakiipata,” alisema Prof. Mbarawa.
Pia aliahidi kuwa serikali utahakikisha barabara zote nchini zinapitika bila vikwazo vya aina yoyote.Nao wananchi waliojitokeza katika ziara hiyo, mbali na kuishukuru serikali kuwaletea maendeleo katika maeneo yao, waliiomba kupewa maeneo ya kujihifadhi wakati wakitafuta makazi ya kudumu.
Comments
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA