WAONYWA MGAWO WA UMEME TANESCO

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kuweka utaratibu wa kutoa taarifa wanapokata umeme ili kuondoa minong’ono kuwa nchi imeingia kwenye mgawo.

Alitoa agizo hilo wakati alipotembelea kituo cha kufua umeme cha Mtera.Alisema Watanzania wengi kilio chao ni taarifa, mwananchi wa kawaida akiona umeme umekatika anajua ni mgawo, lakini wanatakiwa kufahamu umeme unakatika kutokana na matengenezo na marekebisho mbalimbali.

“Pamoja na jitihada kubwa zinazofanyika katika matengenezo na kurekebisha miundombinu mbalimbali, Watanzania hoja yao ni kukatika kwa umeme, tukae kwa pamoja na kuboresha utoaji wa taarifa, watu wanalalamika wanaunguliwa na vitu vyao hii ni changamoto lazima tuifanyie kazi,” alisema.

Aidha, alisema taarifa hizo lazima zieleze umeme umekatika kwa sababu gani, utawaka saa ngapi na utarejea muda gani.

Aliwataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa mto Ruaha, kutunza mazingira kwa kuwa wengi wao wanatumia vibaya maji na kusababisha uharibifu wa mazingira.

Alisema lazima juhudi zifanyike ili kuzuia uharibifu huo ili bwawa na Mtera lipate maji kwa kina kinachostahili.Meneja wa Kituo cha Mtera, John Skauki, alisema mitambo ya kufua umeme iko katika hali nzuri na sasa mpango wa matengenezo kwa kuzingatia umri wa mitambo wa miaka 28 umeanza.

Alisema kwa sasa ujazo wa maji katika bwawa hilo kina cha juu ni mita 698.5 na kina cha chini ni mita 690.Alisema bwawa hukusanya maji kutoka mito ya Ruaha Mkuu, Ruaha mdogo na Kisigo.
Alisema kutokana na mvua za kutosha mwaka 2016 kina cha juu cha maji katika bwawa kilifikia mita 697.4 juu ya usawa wa bahari.

Aidha, kina kilishuka kutokana na ufuaji wa umeme pamoja na mtiririko wa chini ya wastani wa mita za ujazo 75 kwa sekunde.

Alisema kina cha maji hadi kufikia Desemba 3, mwaka huu ni mita 691.04 juu ya usawa wa bahari.Hata hivyo, alisema juhudi za kunusuru bonde la mto Ruaha ziwe endelevu maana hicho ndicho chanzo cha kuaminika cha kufanya Bwawa la Mtera kuwa na maji ya uhakika na hivyo kuleta uhakika wa ufuaji umemekatika kituo cha Mtera na Kidatu mwaka mzima.

Naye, Meneja Mwandamizi wa Tanesco, Kanda ya Kati, Athanasius Nangali, alisema wamepokea maelekezo katika suala la uboreshaji wa utoaji wa taarifa.

“Tulishaanza kupita mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kukusanya namba za simu ili kama kutakuwa na matengenezo tuwajulishe kwa namba za simu,” alisema Nangali.

Comments