YANGA walikuwa makini wakiangalia matukio yote ya Jumapili iliyopita wakati watani wao Simba walipofanya maamuzi ya kihistoria kwa kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu yao, kisha Wana Jangwani hao wakasema nao wanafufua mipango yao ili wasije wakaachwa nyuma.
Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Mhandisi Clement Sanga, amewaambia Simba kuwa wao si wa kwanza kuanzisha mfumo huo, kwani klabu yake ilikuwa ya kwanza na mpaka sasa kampuni hiyo ipo, ingawa kuna mambo machache yanatakiwa kufanyiwa kazi.
Sanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB), alisema Yanga ina kampuni halali ambayo ilishapitishwa katika mikutano ya klabu yao na sasa kwa kuwa serikali imekubali timu hizo zibadilike, basi watafufua mambo yao.
Alisema Yanga anayoingoza yeye itarudisha mipango hiyo kwa kufuata kile ambacho serikali inataka kifanyike kwa usahihi. Katika hilo alisema Kamati ya Utendaji yao itakutana Desemba 13 kujadili.
“Ni jambo la wazi mpira wa sasa unahitaji fedha, na mpango mzuri ni huo wa uwekezaji mkubwa,” alisema.
Wakati Sanga akisema hivyo, baadhi ya wanachama wa Yanga wamefungukia mchakato huo.
Edwin Kaisi amesema mabadiliko ni hatua isiyoweza kurukwa na kwamba ni wakati muafaka kwa wanachama wenzao waliokuwa wakipinga, kuangalia walichokifanya Simba.
Mwanachama mwingine, Said Bakari ‘Said Mosha’ yeye alisema: “Kwanza niwapongeze Simba kwa hatua yao, nasi Yanga tubadilike.”
NYOTA WAKUNWA
Mabadiliko ya Simba yamewagusa hadi nyota wa zamani wa Yanga, ambao wameipa tano Simba.
Katibu wa zamani wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kama kuna jambo la maana Simba wamefanya, basi ni kukabidhi timu kwa wenye fedha.
“Hili jambo si la kishabiki, linataka elimu ya hali ya juu ili wanachama walielewe,” alisema.
“Mfumo wa hisa ni wa kisasa, unasaidia kupunguza baadhi ya kero zisizo na sababu, mfano mzuri namna wanavyochangishana wanachama wa Yanga na Simba, hayo yatapungua badala yake, kutakuwa na mpango madhubuti,” alisema.
Katibu Mwenezi wa zamani wa Yanga, Abdul Sauko, alisema kuingia kwenye hisa ni mfumo sahihi.
Credit – Mwanaspot
Previous article
Comments
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA